Ancelotti asaini mkataba wa miaka minne Brazil, afichua nia yake
Shirikisho la Kandanda la Brazil (CBF) limetangaza kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa hilo, Carlo Ancelotti amesaini mkataba mpya wa miaka minne utakaodumu hadi Julai 2030.
Mtaalamu huyo wa Kiitaliano ambaye mkataba wake wa awali ulikuwa unaisha baada ya fainali za Kombe la Dunia 2026, sasa atakuwa na jukumu la kuiongoza miamba hiyo ya soka kwenye fainali mbili za Kombe la Dunia za 2026 na 2030.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba mpya, Don Carlo amesema: "Nilipowasili Brazil mwaka mmoja uliopita, nilielewa mara moja nini maana ya mpira wa miguu kwa nchi hii. Mimi na CBF tunataka makubwa zaidi, ushindi zaidi, muda zaidi, na kazi zaidi. Tutasonga mbele pamoja hadi Kombe la Dunia la 2030."
Uamuzi huu unakuja ikiwa ni siku 30 tu kabla ya Brazil kuanza kampeni yao ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco mnamo Juni 13, huku kukiwa na imani kubwa kutoka kwa viongozi wa shirikisho hilo kuwa Ancelotti ndiye mtu sahihi wa kuifikisha timu hiyo kwenye kilele cha soka la dunia kwa mara nyingine.